Klabu ya Arsenal imeanza mapema ujenzi wa kikosi chake tayari kwa msimu ujao wa ligi kuu ya soka nchini England, baada ya kuripotiwa kukamikisha usajili wa beki wa kushoto wa kimataifa wa Bosnia Sead Kolasinac, anayekipiga Shalke 04 ya Ujerumani.
Taarifa kutoka Sky Sports zinasema Kolasinac mwenye umri wa miaka 23, anayetumia vyema mguu wake wa kushoto na mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani atajiunga na Arsenal Julai mosi, ikiwa ni saa chache baada ya mkataba wake na Shalke 04 utakapofikia mwisho, Juni 30 mwaka huu.
Kolasinac amesaini mkataba wa miaka mitano na atakuwa akilipwa mshahara wa pauni 120,000 kwa juma na kuwa mchezaji wa tatu anayevuta mkwanja mrefu zaidi baada ya Mesut Ozil anayelipwa £140,000 na Alexis Sanchez anayelipwa £130,000.
Ujio wa Kolasinac kwenye kikosi cha Arsenal umeanza kuibua maswali juu ya hatima ya mabeki Nacho Monreal na Kieran Gibbs ambao wameshindwa kuonyesha kuyamudu vyema majukumu yao uwanjani.
Kolasinac anaiacha Shalke 04 akiwa ameichezea zaidi ya michezo 115.
Msimu huu Kolasinac ameifungia timu hiyo mabao matatu na kupika/kutengeneza mabao tisa katika michezo 39.