Klabu ya Arsenal imetajwa kuwa kwenye mpango wa kumsajili kiungo kutoka nchini Ubelgiji na klabu ya Manchester United, Marouane Fellaini.
Kiungo huyo ambaye ni sehemu ya kikosi cha Ubelgiji kitakacho kwenda nchini Urusi kwa ajili ya fainali za kombe la dunia, anatarajiwa kuondoka Old Trafford na kuwa mchezaji huru mwishoni mwa mwezi huu, kufuatia uongozi wa Man Utd kushindwa kuafikiana naye kuhusu mkataba mpya.
Mazungumzo kati ya uongozi wa Man Utd na Fellaini yaliyoanza tangu mwanzoni mwa mwezi Mei yameshindwa kuzaa matunda, kufuatia pande hizo mbili kukinzana katika suala la mkataba mpya, ambapo upande wa klabu ulihitaji kumsainisha mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza miezi mingine 12 kama atakuwana kiwango kizuri, ili hali mchezaji alihitaji mkataba wa miaka miwili.
Wakala wa kiungo huyo amesema, tayari klabu kadhaa kutoka Italia na Uturuki zimeoshaonyesha nia ya kutaka kumsajili mchezaji wake, huku Arsenal ya England ikionyesha dhamira ya kutaka kufanya hivyo ili kuboresha kikosi chake kwa msimu ujao.
Msimu uliopita Fellaini aliitumikia Man Utd katika michezo 23 na kufanikiwa kufunga mabao matano na kutoa pasi moja iliyozaa bao.
Fellaini mwenye umri wa miaka 30, alijiunga na Man Utd mwaka 2013 kwa ada ya Pauni milioni 27.5 akitokea Everton, na mshahara wake kwa juma ulikua Pauni 80,000.
Arsenal inapewa nafasi kubwa ya kumnasa Fellaini, kufuatia uwepo wa Sven Mislintat anaeongoza kitengo cha usajili klabuni hapo, huku ikiwa chini ya meneja mpya Unai Emery waliemtangaza Mei 23.
Mislintat alipokua na klabu ya Borussia Dortmund alifanikisha usajili wa wachezaji mashuhuri kama Robert Lewandowski, Shinji Kagawa na Ousmane Dembele, na tangu alipotua huko kaskazini mwa jijini London amesaidia usajili wa mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang aliejiunga na The Gunners mwezi Januari akitokea Ujerumani.
Mislintat atafanya kazi kwa ukaribu na Emery wakisaidiana na mtendaji mkuu Ivan Gazidis, katika harakati za kukiongezea nguvu kikosi cha Arsenal kwenye kipindi hiki cha usajili kuelekea msimu wa 2018/19.