Arsenal imeonyesha kuwa tayari kumuachia kwa mkopo kiungo kutoka nchini England Jack Wilshere kwa masharti maalum ambayo kama yatakubaliwa na klabu itakayoonyesha nia ya dhati ya kumsajili kabla ya dirisha la usajili kufungwa, basi biashara hiyo itafanyika.

Wilshere ameshindwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Arsenal tangu mwanzoni mwa msimu huu, kufuatia kuwa na wakati mgumu wa kurejesha kiwango chake ambacho kiliathiriwa na majeraha ya goti aliyoyapata msimu uliopita.

Arsenal wanalazimika kusubiri ndani ya siku mbili zilizosalia kabla ya mwisho wa usajili katika kipindi hiki, ili kupata muda wa kupokea maombi kutoka kwenye klabu yoyote ambayo itakua tayari kuafiki masharti maalum ambayo yataafikiwa.

Masharti ambayo Arsenal waliyoyaweka kabla ya kukubali kumuachia Wilshere aondoke kwa mkopo, ni kuhakikisha anacheza katika kikosi cha kwanza cha klabu itakayomsajili ili kumuwezesha kulinda kipaji chake cha soka.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24, ameachwa kwenye kikosi cha wachezaji waliotajwa kuunda kikosi cha timu ya taifa ya England ambacho kimeanza kambi ya kujiwinda na mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 dhidi ya Slovenia.

Hata hivyo Sam Allardyce alionyesha kusikitishwa na hatua ya kumuacha Wilshere kwa sababu za kutokua na kiwango cha kutosha, ambapo alisema kwa sasa hatoweza kuwa na mchezaji huyo japo anatambua mchango wake ambao amekua akiutoa katika timu hiyo.

“Kwa sasa Jack hajafikia kiwango cha kuitwa timu ya taifa kutokana na matatizo ya majeraha yaliyokua yakimkabili, Natumai wakati mwingine huenda nikamuita na hii itategemea na mustakabali wa kucheza kwake katika kikosi cha kwanza cha klabu yake ya Arsenal,”

“Endapo Jack Wilshere atapata nafasi ya kucheza kila mwishoni mwa juma, atafanikiwa kurejea katika kiwango chake kama ilivyokua zamani,¬†lakini kwa sasa imekua ngumu kufikia lengo hilo.” Alisema Sam Allardyce

Wilshere alikosa sehemu kubwa ya msimu wa 2015-16, hatua ambayo ilimsababishia meneja wa Arsenal (Arsene Wenger) kumsajili kiungo kutoka nchini Misri, Mohamed Elneny mwezi Januari na kisha alimsajili kiungo mwingine kutoka nchini Uswiz mwezi Juni Granit Xhaka.

Joe Hart Kufanyiwa Vipimo Vya Afya Mjini Turin-Italia
Hamisi Kiiza Amfuata Mrisho Ngassa Afrika Kusini