Kikosi cha washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London (Arsenal), kimerejea jijini humo kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu ya soka nchini England.
Arsenal wamerejea jijini London wakitokea Singapore walipokuwa wamekwenda kwa ajili ya michezo ya kirafiki dhidi ya Atletico Madrid na PSG ambayo ilichezwa juma lililopita.
Wakati The Gunners wakirejea jijini humo, kiungo kutoka nchini Uruguay Lucas Torreira amejiunga rasmi na wachezaji wenzake na kufanya mazoezi yake ya kwanza, baada ya kusajiliwa na klabu hiyo akitokea Sampdoria ya Italia.
Kiungo huyo alifika jijini London majuma mawili yaliyopita kukamilisha taratibu za usajili wake, na kisha alirejea nchini kwao Uruguay kwa mapumziko, baada ya kumaliza majukumu ya kuitumikia timu ya taifa lake kwenye fainali za kombe la dunia.
Arsenal itafanya mazoezi jijini London kwa siku kadhaa, kisha itaelekea mjini Dublin – Jamuhuri ya Ireland, kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Chelsea ambao umepangwa kuunguruma mwishoni mwa juma hili kwenye uwanja wa Aviva.
Mchezo huo utakua wa kwanza kwa mameneja wa klabu hizo mbili (Unai Emary na Maurizio Sarri) kukutana kwa mara ya kwanza tangu walipopewa majukumu ya kuvinoa vikosi vya klabu hizo za jijini London.