Aliyekua meneja wa klabu ya Arsenal ya England Arsene Wenger, amekanusha taarifa za kuwa mbioni kuchukua nafasi ya ukuu wa benchi la ufundi la AC Milan, kama ilivyoripotiwa jana katika vyombo habari ulimwenguni kote.
Wenger amesema taarifa hizo sio za kweli, na alipoziona zinasambaa kwa kasi zilimshutua sana.
Jarida la France Football lilisambaza taarifa za babu huyo kutoka nchini Ufaransa, kwa kudai amefanya mazungumzo na uongozi wa AC Milan, ambao kwa sasa umeonyesha kutokua na imani na meneja wao Gennaro Gattuso.
Wenger amekanusha taarifa hizo, alipohojiwa na kituo cha televisheni cha beIN SPORTS usiku wa kuamkia leo, ambapo alisema waliosambaza taarifa za yeye kuwa mbioni kuelekea mjini Milan kikazi, hafahamu walikua na kusudio gani.
“Kitu kikubwa ninachotaka kusema ni kwamba, taarifa hizo hazina ukweli na waliozisambaza sijui walikua na maana gani,” alisema Wenger aliyekinoa kikosi cha Arsenal kwa muda wa miaka 22 mfululizo.
“Laiti kama ingelikua ukweli, ningekuja hapa nikawaambia, lakini sio ukweli na ndio maana ninakanusha kwa nguvu zote.”
“Siwezi kuishi katika misingi ya habari za tetesi, siku zote nimekua muumini wa ukweli na uhalisia wa jambo lolote katika maisha yangu. Kwa sasa sina lingine la zaidi ya kazi yangu ninayoifanya katika kituo hiki cha beIN SPORTS,” aliongeza mzee huyo mwenye umri wa miaka 69.
Tangu Wenger alipoondoka Arsenal mwezi Mei mwaka huu, bado hajapata kazi kwenye klabu yoyote, na taarifa zilizosambazwa jana zilidai huenda angerejea katika shughuli za ukufunzi wa soka mwezi Januari mwaka 2019.