Mashabikiwa wa Arsenal wanamshukuru nguli Arsene Wenger kwa ushauri aliompa Bukayo Saka kumfanya winga huyo azidi kuwa moto zaidi ndani ya uwanja.

Imeelezwa kwamba Kocha huyo wa zamani wa Arsenal, Wenger alimpa ushauri winga huyo wakati walipokutana kwa mara ya kwanza mwaka jana, wakati The Gunners ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham United, Desemba 2022.

Makamu mwenyekiti wa Arsenal, Tim Lewis alifichua kile kilichozungumzwa wakati Wenger alipokutana na Saka.

Lewis alisema: “Ilikuwa kitu kizuri Arsene kuingia vyumbani. Bukayo (Saka) hakuwa anamfahamu, lakini alimwita bosi kwa haraka sana. Alisema, ‘Bosi, vipi naweza kuwa bora?’ Arsene alimjibu kwa kumwambia, ‘Nadhani utumie vizuri mguu wako wa kulia zaidi”.”

Baada ya kufichuka kilichozungumzwa, Wenger alipokutana na Saka, mashabiki wa Arsenal wamefurahia na kila mmoja kusema lake, lakini kubwa wakisifu ushauri wa mkongwe huyo katika kumfanya staa wao kuendelea kuwa moto ndani ya uwanja.

Saka aliibukia kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal baada ya Wenger kuondoka, hivyo hakupata nafasi ya kucheza mzee huyo wa kifaransa.

Katika msimu uliopita, Saka mwenye umri wa miaka 21, alifunga mabao 15 na kuasisti 11 kwenye kikosi cha Arsenal. Ubora wake ulimfanya abambe dili jipya la kubaki kwenye kikosi hicho hadi majira ya kiangazi mwaka 2027.

Jurgen Klopp asaka mkwanja wa usajili Liverpool
Namungo FC yasajili mshambuliaji mzoefu