Kwa kuonesha amedhamiria kuendelea kufanya kazi barani Ulaya hata kama hatosaini mkataba mpya wa kuendelea kukinoa kikosi cha Arsenal mwishoni mwa msimu huu, Arsene Wenger, ameripotiwa kukataa ofa ya kwenda nchini China.
Gazeti la The Independent limeripoti taarifa za meneja huyo kutoka nchini Ufaransa kukataa ofa hiyo, ambayo ingemuwezesha kuwa meneja anaelipwa mshahara mkubwa ziadi duniani.
Bila kutaja klabu iliyowasilisha ofa mikononi mwa Wenger, gazeti la Independent limeeleza kuwa, babu huyo ameahidiwa kulipwa Pauni milioni 30 kwa mwaka endapo atakubali kuelekea nchini China kupeleka ujuzi wake wa ukufunzi wa soka.
Mshahara wa Pauni milioni 30, ni mara ya mbili ya mshahara wa meneja wa Man City Pep Guardiola, ambaye kwa sasa ndiye analipwa kiasi kikubwa kuliko mameneja wengine nchini England.
Kukataa kwa mzee huyo wa kifaransa, kunaaminiwa huenda akawa na mpango wa kubaki Emirates Stadium, kutokana na uongozi wa Arsenal kumtayarishia mkataba wa miaka miwili.
Hata hivyo mpaka sasa bado haijafahamika kama mzee huyo yupo tayari kuikubali ofa ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kukinoa kikosi cha Arsenal ama la, japo gazeti hilo limetaja ongezeko la mshahara atakaolipwa endapo ataendelea kubaki Emirates Stadium.
Arsenal wamemuahidi Wenger ongezeko la mshahara la Paundi milioni mbili kutoka Pauni milioni 8 hadi Pauni milioni 10.