Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger ameingilia kati mazungumzo ya viongozi wa klabu hiyo na wale wa Man city, na kupinga ofa ya Pauni milioni 60 pamoja na mshambuliaji Raheem Sterling ili kukamilisha uhamisho wa Alexis Sanchez kuelekea Etihad Stadium.
Wenger amepinga dili hilo kwa kusema hana mpango na Sterling kwa sasa, na kama itashindikana ni bora Man City watoe kiasi kamili cha pesa ambacho kitatajwa na The Gunners, la sivyo anaona ni bora akaendelea kuwa na Sanchez kwa msimu huu na kisha kumuachia kama mchezaji huru mwishoni mwa msimu huu.
Wenger amesema kama Man City wanataka kufanya biashara ya usajili wa Sanchez kihalali, itawalazimu kutoa kiasi cha pesa sambamba na mshambuliaji wao kutoka nchini Argentina Sergio Aguero.
Hata hivyo mpaka sasa meneja wa Man City Pep Guardiola hajazungumza lolote kuhusu ombi hilo la Aresen Wenger, na inasubiriwa kitakachoamuliwa, baada ya pande hizo mbili kumaliza mazungumzo hii leo.
Sanchez yu njiani kuondoka Arsenal, baada ya kugoma kusaini mkataba mpya, kufuatia mkataba wake wa sasa kutarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.