Pamoja na kukubali kutupwa nje ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa kuchapwa mabao kumi kwa mawili, meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger amepingana na waandishi wa habari kwa kusema haamini kama klabu hiyo inahitaji mabadiliko kwa sasa.

Wenger alibanwa kwa maswali na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo kumalizika huko kaskazini mwa jijini London, lakini alionyesha ujasiri wa kuyajibu.

Moja ya maswali alioulizwa mzee huyo kutoka nchini Ufaransa ni kuhusu mabadiliko ambayo huenda yakainusuru klabu hiyo kwa kushindwa kufanya vizuri katika michezo ya ligi ya England, na ile ya kimataifa, lakini akasisitiza hakuna haja ya kufanyika mabadiliko.

“Unamaanisha nini? Alihoji Wenger baada ya kuulizwa swali hilo.

“Nafikiri klabu ipo katika muhimili mzuri, japo tunapita katika kipindi kigumu, lakini mambo yatakaa sawa.

“Tunachotakia kufanya kwa sasa ni kujitahidi kubadilisha matokeo na kuwafurahisha mashabiki wetu.”

Hata hivyo Arsenal itacheza mchezo ujao dhidi ya klabu ya Lincoln City inayoshiriki madaraja ya chini nchini England katika michuano ya kombe la FA mwishoni mwa juma hili.

“Tutacheza mchezo wa robo fainali ya kombe la FA jumamosi, tunataka kuelekeza akili na fikra zetu kwenye mchezo huo,”

“Tunataka kufanya kazi yetu kikamilifu ili tufanikishe mpango wa kusonga mbele, na si kufikiria mambo yaliyopita kwa kushinikiza mabadiliko.” Aliongeza Wenger.

Ange Postecoglou Awaita Tim Cahill, Tomi Juric
Jose Mourinho Aichimba Mkwara Real Madrid