Maneja wa Arsenal Mikel Arteta, amesisitiza kuwa, hivi sasa wako bize kuangalia ni namna wanashinda kila mchezo bila kujali maneno ya wapinzani wao akiwemo Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola.
Juzi Jumapili (Machi 12) Arsenal iliibuka na ushindi wa mabao 0-2 dhidi ya Fulham katika mchezo wa Ligi Kuu ya England wakati staa wao, Gabriel Jesus akirejea uwanjani.
Arteta amesema hayo baada ya Guardiola kunukuliwa akisema kwamba, Man City kupata kwake ushindi kunaiongezea presha zaidi Arsenal.
Kocha huyo amesema: “Sijui ni nini, lakini huwa tunajadili vitu vyetu na kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.”
“Tunajadili vitu gani vya kufanya mazoezini, hii ni katika kuhakikisha tunakuwa bora, hilo ndiyo lengo letu kila siku. Hatutaki kusikiliza wengine wanasema nini, tunachofanya ni kushinda michezo yetu.”
Kuhusu ubingwa, Arteta amesema: “Hicho kinaweza kuwa kitu cha kipekee. Watu wengi wanakuja hapa na wamekuwa wakiwekeza nguvu zao kuhakikisha kila kitu kinaenda vizuri kwa kupata matokeo bora hasa kwa kila mchezo ulio mbele yetu.”
“Matokeo bora kama ambayo tumepata wikiendi yalikuwa muhimu kwetu na kikubwa tumeweza kutoka na clean sheet na tumeendelea kuwa katika nafasi nzuri.”
Kwa sasa, Arsenal ipo kileleni mwa msimamo mwa Ligi Kuu ya England ikiwa na alama 66, ikifuatiwa na Manchester City yenye 60.