Kocha Mkuu wa Arsenal Mikel Arteta, amewapogeza wachezaji wake kwa kiwango kizuri walichokionyesha katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Manchester City, juzi Jumapili (Oktoba 08).

Arsenal ilipata ushindi huo katika mchezo wa Ligi Kuu ya England uliopigwa Uwanja wa Emirates, kaskazini mwa jijini London.

Bao la Mbrazili Gabriel Martinelli dakika ya 86, liliipa Arsenal ushindi huo mnono na kuipandisha hadi nafasi ya pili, ikiwa na pointi 20 sawa na kinara Tottenham Hotspur.

Ushindi huo umeifanya Arsenal kuvunja mwiko wa kutoifunga Man City katika ligi hiyo kwa miaka minane.

Mara ya mwisho kwa miamba hiyo kutoa London Kaskazini kuifunga Manchester City katika ligi, ilikuwa Desemba mwaka 2015.

“Unaweza kuhisi imekuwa miaka mingi bila ya kuwafunga. Juzi nafikiri tumeifunga timu bora zaidi duniani bila ya shaka,” alisema.

Arteta alisema kikosi chake kimeifunga Man City katika njia bora kwani kuna wakati ilipata shida uwanjani na wakati mwingine ilionyesha hamu, dhamira na imani ya kweli kupata pointi tatu.

“Tumefanya katika njia bora kwa sababu kuna nyakati ambazo tuliteseka na kuna wakati ambao tulionyesha hamu, dhamira na imani ya kweli kuwafunga,” alisema.

“Hivyo nina furaha sana. Inatuma ujumbe kwa timu kuendelea kuamini katika kile wanachokifanya kwa sababu ni kundi la wacheząji wazuri,” aliongeza.

Kocha huyo alisema matunda ushindi huo yametoka na kikosi hicho kujifunza kupitia makosa ilyoyafanya msimu uliopita ilipokutana na Man City.

Katika Ligi Kuu England msimu uliopita, Arsenal ilipoteza nyumbani kwa mabao 3-1, kabla ya kufungwa ugenini mabao 4-1.

Kocha Mtibwa Sugar ajitetea
Rais Samia atunukiwa PhD India, aipeleka kwa Watoto