Vinara wa ligi ya Ufaransa AS Monaco wapo tayari kumpa ruhusa ya kuondoka kiungo wao kutoka nchini Ureno Bernardo Silva utakapofika wakati wa usajili wa majira kiangazi.
Gazeti la michezo la Ufaransa la L’Equipe limeeleza kuwa, uongozi wa AS Monaco umefikia maamuzi ya kumpa uhuru wa kuondoka kiungo huyo, ili kutoa nafasi kwa mpinzani wake Thomas Lemar kusalia klabuni hapo.
Wawili hao wamekua na upinzani wa kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha AS Monaco, hali ambayo ilisababisha mchakato wa mmoja wao kufikiria kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Uongozi wa AS Monaco umeona ni bora kumuachia Silva ambaye ana thamani kubwa kwa sasa, na waendelee kubaki na Lemar ambaye wanaamini atawafaa kwa msimu ujao wa ligi ya Ufaransa na ile ya barani Ulaya.
Tayari klabu ya Barcelona, Chelsea na Manchester United zimeshaingia katika vita ya kumuwania Silva, na huenda hali hiyo ikaongeza thamani ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22.
Silva alisajiliwa moja kwa moja na AS Monaco mwaka 2015 baada ya kujiunga na vinara hao wa Legue 1 kwa mkopo 2014, akitokea nchini kwao Ureno alipokua akiitumikia klabu ya Benfica.