Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amesema wameanza maandalizi ya kuelekea mchezo wa Mzunguuko wanne wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya AS Real Bamako ya Mali.
Young Africans itacheza mchezo wake wa pili Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Jumatano (Machi 08) nyumbani kwa kuikaribisha AS Real Bamako ya Mali, huku ikichagizwa na ushindi walioupata dhidi ya TP Mazembe mwezi uliopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kocha Nabi amesema lengo kubwa kuelekea mchezo huo ni kusaka ushindi utakaowaweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu Hatua ya Robo Fainali, japo anatambua wapinzani wao watataka kufanya hivyo ili kujinusuru kutokana na nafasi waliopo hivi sasa katika msimamo wa Kundi D.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema mchezo uliopita dhidi ya AS Real Bamako walikaribia kupata ushindi ugenini, lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo, ila safari hii wamejipanga kurekebisha makosa hayo ili kuzinasa alama tatu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Matarajio yetu katika mchezo uliopita yalikuwa ni kuweza kushinda ugenini, lakini tuliambulia matokeo ya sare ambayo kimahesabu hayakuwa mabaya sana kwetu, kwa sababu hata wenzetu walijitahidi kupata bao la kufutia machozi na walifanikiwa.”
“Dhumuni kubwa la mchezo wetu unaofuata dhidi ya AS Real Bamako ni kuhakikisha tunashinda katika Uwanja wa nyumbani kama tulivyofanya kwa TP Mazembe, nina uhakika inawezekana kwa sababu wachezaji wangu wameonyesha kuwa tayari kwa hilo.”
“Nafahamu haitakuwa rahisi kwa sababu hata wapinzani wetu watahitaji kupata ushindi, kwa kuwa hawana cha kupoteza kutokana na mtazamo wa Kundi ulivyo sasa, kwa hiyo tutapaswa kucheza kwa malengo huku tukiwa na tahadhari kubwa sana.” amesema Nabi
Hadi sasa Msimamo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika US Monastir ya Tunisia inaongoza ikiwa na alama 07, ikifuatiwa na Young Africans iliyojikusanyia alama 04, TP Mazembe inashika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 03 na AS Real Bamako inaburuza mkia wa Kundi hilo kwa kuwa na alama 02.