Beki wa kati kutoka nchini Morocco Medhi Amine El Mouttaqi Benatia, huenda akaachana na mabingwa wa soka nchini Italia Juventus, itakapofika mwezi Januari mwaka 2019 (Dirisha dogo la usajili ).
Mijadala kadhaa tayari imeshajadiliwa katika vikao vya wakubwa wa klabu hiyo ya mjini Turin kuhusu kuuzwa kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 31, na asilimia kubwa inaonesha huenda akaruhusiwa kuondoka.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya Tuttosport klabu za AS Roma na AC Milan zote za Italia, zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili beki huyo ambaye kwa sasa ana wakati mgumu wa kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Juventus.
Tangu aliporejeshwa beki Leonardo Bonucci mwanzoni mwa msimu huu akitokea AC Milan, Benatia amekua na changamoto kubwa ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
AS Roma wametajwa kutenga dau la Pauni milioni 20, kama ada ambayo wanaamini itatosha kufanikisha usajili wa beki huyo, ambaye alijiunga na Juventus mwaka 2017 akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich.
Kwa upande wa AC Milan bado haijathibitika wametenga kiasi gani cha fedha ambacho wanataka kukitumia kwenye usajili wa beki huyo.
Msimu wa 2013–2014 Benatia aliitumikia AS Roma kwa kucheza michezo 33 na kufunga mabao matano, na endapo atafanikisha mpango wa kusajiliwa na klabu hiyo, hatokua na mazingira ya ugeni, tofauti na AC Milan.
AS Roma ndio walimuuza beki huyo kwa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich mwaka 2014.