January,31,2019 Young Africans na Biashara United Mara zilikutana kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya Azam Sports Federation Cup.

Mchezo huo kati ya Young Africans dhidi ya Biashara United Mara ulichezwa kwenye uwanja wa Benjamin William Mkapa jijini Dar-es-salaam na dakika 90 zilimalizika kwa sare ya mabao 2-2 kabla ya kwenda kwenye hatua ya mikwaju ya penati.

Biashara United Mara walitangulia kupata goli la kwanza ambalo lilifungwa na Waziri Junior dakika ya 2 kwa mkwaju wa penati.

Mkwaju huo ulipatikana baada ya beki wa Young Africans Andrew Vicent Chikupe kumfanyia madhambi mchezaji wa Biashara United Mara, George Makang’a.

Dakika ya 8 Young Africans walisawazisha goli hilo kupitia kwa Hamisi Tambwe ambaye alipiga penalty iliyotokana na mchezaji wa Young Africans Ibrahim Ajibu kuanguka kwenye eneo la 18 la BUM baada ya purukushani baina yake na beki wa Biashara United Mara Lenny Kissu.

Dakika ya 40 Innocent Edwin aliifungia Biashara United Mara goli la pili safi kabisa akimuacha kipa wa Young Africans Ramadhani Kabwili akiwa hana la kufanya.

Papatu papatu baina ya miamba wa kanda ya ziwa na vijana wa mitaa ya Jangwani iliendelea ambapo dakika ya 73 Mrisho Ngasa alipiga pasi kwa Gadiel Michael ambaye aliachia mpira uliomkuta Heritier Makambo akafanikiwa kusawazisha.

Dakika 90 zilimalizika kwa matokeo ya Young Africans 2-2 Biashara United Mara na ikafuata hatua ya matuta.

Biashara United Mara ilianza kupiga tuta la kwanza kupitia Lenny Kissu ambaye alifunga na Young Africans alianza Heritier Makambo na yeye alifunga.

George Makang’a alipiga mkwaju wa 2 akaweka mpira kambani huku Paul Godfrey na yeye akiwafungia Young Africans.

Derick Musa alifunga mkwaju wa 3 huku Ibrahim Ajibu na yeye alifunga kwa upande wa Young Africans.

Biashara United Mara walikosa mkwaju wa 4 uliopigwa na Tariq Seif Kiakala huku Young Africans wakipata kupitia Thaban Kamusoko.

Kauswa Bernard alihitimisha mikwaju ya BUM na alifunga goli zuri huku Matheo Anthony akifunga mkwaju wa Young Africans na mchezo ulimalizika.

IMEANDALIWA NA,

IDRISA SECHAMBO.

Tundu Lissu auchambua utawala Afrika Mashariki
Biashara Utd: Tupo tayari kuivaa Young Africans