Uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa unahitaji ushindi kwenye mchezo wao wa Hatua ya Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Azam FC utakaopigwa mkoni Mtwara katika Uwanja wa Nangwanda, Jumamosi (Mei 6).
Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ imetoka kufungushiwa virago na Wydad AC kwenye hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Penati 4-3 baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC Ahmed Ally amesema kuwa wanatambua wengi hawajapenda matokeo hayo lakini imeshatokea kikubwa ni kusonga mbele.
“Wachezaji wetu walijitoa na kupambana lakini ukatili wa matokeo ya mpira umetufanya tuishie Robo Fainali.”
“Tunarejea kwenye michuano ya ndani na focus (matazamio), yetu kushinda mechi zetu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, tunataka kushinda dhidi ya Azam FC baada ya kumalizana na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu unaopigwa leo hapa Lindi.”
“Tunajua kwamba ili tuweze kwenda hatua ya Fainali lazima tupate matokeo mazuri kwenye mchezo wetu.”
“Bado nafasi ipo na tuna mechi ambazo tunapaswa kucheza wachezaji wetu wanajua umuhimu wa mechi hizo na watapata muda wa kupumzika na kujiandaa kuwakabili wapinzani wetu,” amesema Ahmed Ally