Musa Kitambo ambaye ni baba mzazi wa kijana aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mwanaye wa kumzaa, amesherehekea uamuzi huo wa mahakama.
Mzee huyo ameelezea furaha yake mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Masasi kutoa hukumu hiyo dhidi ya mwanaye Ally Katambo mwenye umri wa miaka 30 ambaye alikutwa na hatia ya kumbaka mwanaye wa kike mwenye umri wa miaka 11.
“Mambo kama haya sisi ndio tunayaona siku hizi, zamani hayakuwepo kabisa. Kwa hili mimi ninaipongeza Serikali na Mahakama wametenda haki kabisa,” Nipashe linamkariri Mzee Kitambo.
Mzee huyo alieleza kuwa aliumizwa na kitendo hicho alichokifanya mwanaye dhidi ya mjukuu wake wa kike, kwa kile anachoamini kuwa ni msukumo wa imani za kishirikina baada ya kudanganywa na mganga kuwa ni moja ya sharti la kupata utajiri badala ya kufanya kazi.
Alisema kuwa siku aliyopewa taarifa kuwa mwanaye huyo amembaka mjukuu wake, alipoteza fahamu kutokana na mshtuko. Aliongeza kuwa hata alipoenda kumuona katika hospitali ya Mission ya Ndanda alikuwa akipoteza fahamu mara kadhaa.
Alisema kuwa adhabu aliyopewa mwanaye ya kifungo cha miaka 30 jela ni ya haki ili iwe fundisho kwa watu wengine.