Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP limesema takriban asilimia 40 ya watu wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia wanakabiliwa na uhaba wa chakula.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo hali ya maafa katika jimbo la Tigray ilianza baada ya mashirika ya misaada kulazimika kupunguza kazi zao kutokana na ukosefu wa petroli na mahitaji mengine ya ugavi. Wafanya kazi wa mashirika ya misaada wanalazimika kutembea kwa miguu ili kwenda kutoa misaada. Shirika la WFP limesema mapigano mapya pia yamesababisha njia za kupelekea misaada zipungue.
Tathmini ya Umoja wa Mataifa imebainisha kwamba watu milioni 4.6 wanaowasilisha asilimia 83 kwenye jimbo la Tigray hawana uhakika wa kupata chakula na watu wapatao milioni mbili kati ya hao wamo katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na baa la njaa.
Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Mashariki, Michael Dunford ametoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa njaa katika mikoa jirani ya Amhara na Afar, ambayo amesema imeathiriwa sana na mapigano katika miezi ya hivi karibuni.
Dunford amesema shirika la WFP linafanya kila linalowezekana kuhakikisha misafara yake ya chakula na dawa inafika kwenye maeneo yaliyomo kwenye hali ngumu kutokana na mapigano. Mkurugenzi wa WFP amesema pande zote katika mgogoro huo zinahitaji kukubaliana na kusitisha mapigano ili misaada na mahitaji mengine iweze kuwafikia mamilioni ya watu wanaokumbwa na njaa.
Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulisema usambazaji wa chakula katika jimbo Tigray umefikia kiwango cha chini kabisa na utapiamlo unaendelea kuongezeka katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia.