Mashabiki na Wanachama wa Young Africans wameombwa kuwa na subra ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22, licha ya timu yao kuendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa zaidi ya alama 10.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 56, ikifuatiwa na Mabingwa watetezi Simba SC yenye alama 42, hali ambayo inaendelea kutoa nafasi ya kipekee kwa klabu hiyo Kongwe Afrika Mashariki na Kati kulisogelea taji msimu huu.
Ombi hilo kwa Mashabiki na Wanachama wa Young Africans limetolewa na Msemaji wao Haji Sunday Ramadhan Manara alipozungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Jumatatu (Mei 09), ambao utawakutanisha na Tanzania Prinons, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Manara amesema suala la Ubingwa bado kwa klabu ya Young Africans, lakini wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo kwa asilimia 90, akiacha asilimia 10 za kushindwa kufikia lengo hilo.
Amesema Wanachama na Mashabiki wanapaswa kuendelea kuwa kitu kimoja na timu yao katika kipindi hiki, ili kuendelea kulisogelea taji la Ligi Kuu ambalo kwa misimu minne mfululizo lilichukuliwa na Simba SC.
“Bado hatujashinda ubingwa wa Ligi Kuu, lakini nafasi ya kutwaa ubingwa huu ni asilimia 90, yaani asilimia 10 ndio nafasi ya kuukosa ubingwa huu, lakini kwa uhakika tupo zaidi ya asilimia 90, kwa hiyo ubingwa upo kwenye mikoni yetu.”
“Tukiamua wenyewe tusiuchukuwe hatutauchukua, lakini tukiamua tutashinda, hivyo tushirikiane, tupambane tukashinde michezo yetu iliyobaki.”
“Hatuzungumzii Unbeaten, ninazungumzia Ubingwa, tutashinda msimu huu, hizi nyingie kutoka sare, sijui nini, ikitokea tumefungwa bado Young Africans itakua Bingwa Insha Allah, hatuna shaka na hilo. Ingawa haitutengenezei kujiamini kupita kiasi, na hakuna mwanayanga kukubali mpaka tushinde ubingwa wenyewe, yaani tusilale.” amesema Manara