Askari magereza Faustine Masanja anashikiliwa na polisi kwa kumuua askari mwenzake Ombeni Mwakiyani kwa kumpiga risasi kichwani chanzo kikiwa wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Arusha, Charles Mkumbo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea leo majira ya asubuhi wakati wakiwa kazini kwenye gereza la mkoa la Kisongo.

Mmoja wa mashuhuda tukio hilo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake na kuandikwa amesema kuwa askari Masanja alimpiga risasi mwenzake wakiwa wanawapakia mahabusu kwenye gari kwa ajili ya kuwapeleka kwenye mahakama mbalimbali za mkoani hapa kwa ajili ya kusikiliza kesi zao.

“Masanja alikuja akampiga Ombeni risasi ya kichwa kwa nyuma ikatokea usoni alipomaliza akatupa silaha chini akasema sikimbii nikamateni kwa kuwa najua nimeua,” alisema shuhuda huyo.

Hata hivyo baadhi ya askari magereza ambao hawakuwa tayari majina yao kuandikwa walidai kuwa Ombeni na Masanja wake zao ni ndugu hivyo kuna uwezekano kulikuwa na mgogoro wa kifamilia.

Aidha Kamanda Mkumbo amedai kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi.

 

 

Azam U-11, U-13 kushiriki Chipkizi Cup
Video: Mbunge mwingine aitosa Chadema