Jeshi la polisi nchini limemfuta kazi Konstebo wa Polisi, Ramadhani Said mwenye namba G.2308 ambaye alionekana kwenye video akiwa amevalia sare za jeshi hilo huku akisifia pombe haramu aina ya gongo.
Jeshi la Polisi limemekuwa likipiga vita matumizi ya gongo na kukamata watengenezaji na watumiaji wa pombe hiyo, lakini kitendo cha askari huyo kuonekana akisifia pombe hiyo hadharani kimetafsiria kama kukiuka maadili ya kazi na kulifedhehesha Jeshi la Polisi.
PC Said alitenda kosa hilo mwaka 2020 na kushitakiwa kijeshi kwa mujibu wa taratibu za jeshi la polisi.
Video ya Said ambaye alikuwa katika ngazi ya kwanza ya ajira ndani ya jeshi la polisi, ilimuonesha akiisifia pombe hiyo na kuipa jina la NIPA (New International Pure Alcohol) na baada ya kusambaa mitandaoni ndipo Rais Samia Suluhu Hassan akakemea kitendo hicho alichokiita ni ukosefu wa maadili.
“Yuko in uniform, kuna raia hapo, angalau utani huo angeufanya ndani yuko police mess anakula na wenzie wameshiba akasimama akafanya huo utani… sijui IGP ulimuona, na kama ulimuona sijui yuko wapi?” Alieleza Rais Samia wakati akihutubia katika hafla ya kufunga mafunzo ya kozi ya uofisa Chuo cha Taaluma ya Polisi.