Afisa wa Jeshi la Magereza nchini Zimbabwe amefunguliwa mashtaka kwa kosa la kumkosea heshima Rais wa nchi hiyo kwa kuandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akimpandisha kiongozi wa upinzani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa na taasisi ya wanasheria ya kutetea haki za binadamu ya Zimbabwe Lawyers for Human Rights (ZLHR), Mamlaka ya Jeshi la Zimbabwe imemfungulia mashtaka John Mhlabera na kwamba kazi yake iko hatarini kwa kudaiwa kumuita ‘Rais’, kiongozi wa upinzani.
Mhlabera anadaiwa kuandika kupitia mtandao wa Twitter kuwa, “Njoo Chiredzi rais wangu.” Hata hivyo, wakati huo aliyekuwa anaingia katika eneo hilo la Chiredzi ambaye anadaiwa kuwa alikuwa anamzungumzia ni kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change –Tsvangirai (MDC-T), Nelson Chamisa na sio Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.
“Mamlaka ya Jeshi la Magereza limeeleza kuwa Mahlabera ameonesha utii kwa Chimisa na kutomtii Rais Mnangagwa. Mamlaka hiyo imedai kuwa kitendo cha Mahlabera ni kumkosea heshima Mnangagwa na kama afisa wa jeshi la magereza hakupaswa kufanya kitendo kama hicho,” imeeleza taarifa hiyo ya ZLHR.
ZLHR imeongeza kuwa imewachagua wanasheria wake wawili kumsaidia Mahlabera atakapofika mbele ya mahakama kusikiliza mashtaka dhidi yake. Imeelezwa kuwa tangu mwaka 2010 zaidi ya kesi 200 zimefunguliwa dhidi ya watu waliomkosea heshima rais wa Zimbabwe.