Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, amesema hakuna askari aliyemzuia mgombea Ubunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro Freeman Mbowe kufanya kampeni.

Sabaya ameeleza hayo leo Oktoba 10 wakati akizungumza na EATV &EA Radio Digital, alipoulizwa alichukuliaje kitendo cha Askari kumzuia mgombea kufanya kampeni huku akidai mgombea huyo hawezi kumshinda mgombea wa chama fulani, ambapo amesema kuwa Askari huyo alifika pale kwa lengo la kuwaweka sawa kwani eneo hilo kulikuwa na mgombea mwingine.

Sabaya ameeleza kuwa video inayosambaa mitandaoni ikimuonesha yeye na Askari wakibishana ni kwa sababu alivunja utaratibu kwa kutaka kufanya kampeni eneo ambalo hakutakiwa kinyume na kanuni za Tume.

“OCD alifika pale kuhakikisha makundi mawili hayahitilifiani na Mbowe alifanya makusudi na aliambiwa aondoke ndiyo mabishano yakatokea, Jeshi la polisi ni chombo cha dola na wanaolitumikia ni binadamu nao wanafika mahali wanakasirika,” amesema Sabaya.

“Aliyevunja taratibu ni huyu mgombea ubunge, naamini Tume nayo itachukua hatua hamuwezi kuweka sheria wenyewe na mnazivunja, halafu mnatafuta huruma nyepesi kwa sababu mmeshindwa kuomba kura, unageuza agenda ya kuomba kura ili ujipatie huruma hiyo haikubaliki kabisa,” ameongeza Sabaya.

Oktoba 7 mwaka huu ilionekana video mitandaoni ikimuonesha Askari Polisi wilayani Hai, akibishana na mgombea ubunge wa jimbo hilo Freeman Mbowe kuhusu ufanyaji wa kampeni huku Askari huyo akidai kuwa Mbowe hawezi kumshinda mgombea wa chama kingine ambaye hakumtaja jina.

CUF Mtwara mjini wafungiwa kampeni siku 10
Ufanyaji wa mazoezi kupunguza magonjwa yasiyoambukiza