Kampala, Uganda. Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi (CDF), Jenerali David Muhoozi, ameamuru kuwakamata na kuwaadhibu askari wote waliowapiga wanahabari waliokuwa wakitimiza jukumu lao la kiuandishi wakati wa maandamano ya kupinga kukamatwa kwa Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Amri hiyo imekuja siku chache baada ya wananchi na jumuiya ya kimataifa kuwashutumu askari wa Jeshi la Ulinzi (UPDF) kwa ukatili na manyanyaso dhidi ya waandishi wa habari ambao walikuwa wakiandika habari za kampeni katika Jimbo la Manispaa ya Arua hivi karibuni, kisha na kisa cha kukamatwa wanasiasa na kuibuka vurugu katika maeneo mengi ya jiji la Kampala Jumatatu.

Taarifa iliyotolewa Jumanne na msemaji wa UPDF Brigeduia Richard Karemire inasema uongozi wa jeshi unalaani ukatili uliofanywa na askari wake.

“Uongozi wa UPDF umefahamishwa kuhusu utendaji kazi usiozingatia weledi wa askari wake waliowasumbua wanahabari waliosambazwa kwa ajili ya kufuatilia operesheni ya pamoja katika jiji Jumatatu ya Agosti 20, 018,” ilisema sehemu ya taarifa Brigedia Karemire iliyosambazwa Jumanne.

“UPDF linapenda kueleza kwamba halijafurahishwa na tabia hiyo iliyofanywa na askari hao binafsi, na kwa sababu hiyo Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi (CDF) ameamuru wakamatwe na waadhibiwe.

Waandishi waliokumbana na mkono katili wa askari wa vikosi vya usalama ni wanahabari wanne wa televisheni ya NTV; Juma Kiirya, Herbert Zziwa, Ronald Muwanga, Ronald Galiwango, na wenzao Julius Bakabaage (NBS), James Akena (Reuters), Samuel Kyambadde (Metro FM) na Richard (Ghetto TV).

Brigedia Karemire alisema: “Wakati tunaomba radhi na kuwapa pole wanahabari waliokumbwa na mkasa huo, tunapenda kusisitiza juu ya dhamira yetu ya kushirikiana kwa dhati na vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yote yaliyoeainishwa na Katiba.”

Aidha CDF Muhoozi aliomba radhi baada ya askari wake kuonekana katika mkanda wa video wakiwapiga waandishi wa habari kwenye maandamano ya kupinga kukamatwa kwa mbunge huyo maarufu kama Bobi Wine Jumatatu.

 

Video: Tunamtambua Prof. Lipumba, Maalim Seif amesimamishwa- Mwinyi
Shilole amkejeli Alikiba kiaina, 'kuna msanii yupo lakini hatuna faida naye'