Abel Paul, Jeshi la Polisi – Dar es Salaam.
Askari Wanawake wametakiwa kuwa mstari wa mbele kushiriki misheni za kulinda amani katika Mataifa yenye changamoto za kiusalama.
Akiongea katika maadhimisho ya 23 ya ulinzi wa amani yaliyofanyika katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi Nchini, kilichopo jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa UN Women Tanzania, Hodan Addou amesema lengo la umoja wa mataifa ni kuwashirikisha Askari Wanawake katika misheni za ulinzi wa Amani.
Amesema, wahanga wakubwa katika machafuko ya kiusalama yanapotokea ni wanawake na watoto huku akisema umoja wa mataifa utaendelea kuweka mazingira bora ya kiusalama kwa makundi hayo.
Kwa upande wake Kamishina wa Utawala na Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi, Suzan Kaganda amesema changamoto kubwa iliyokuwepo siku za nyuma kwa askari wanawake ni uthubutu na utayari wa ushiriki katika ulinzi wa amani tofauti na sasa.
Naye, Balozi wa Swizerland, Didier Chassot amesema katika maswala ya ulinzi wa amani lazima waangalie usawa wa kijinsia ili misheni hizo ziwe na matokeo chanya kwa makundi yote huku akiwaomba kuendelea kuweka mazingira bora ya misheni za kulinda amani.
Kwa upande wa uongozi wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani, umesema umeongeza nafasi za udahili kwa Askari Wanawake katika mafunzo, ili kuongeza uwakirishi wao katika misheni mbalimbali za umoja wa mataifa.