Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kujenga vituo vipya vya askari wa wanyamapori katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja Bungeni jijini Dodoma leo Juni, 30, 2022 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Francis Ndulane.
Ndulane aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kudhibiti tembo wanaoharibu makazi na mashamba katika Kata za Kandawale na Miguruwe ambazo zinapakana na Pori la Akiba Selous.
“Kuna vituo 19 vya askari wanyamapori nchi nzima kwa mwaka huu wa fedha unaoishia lakini kuanzia tarehe 1 Julai 2022 Serikali itaongeza vituo 13 vya askari wanyamapori ili kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu,” Masanja amesisitiza.
Aidha, amesema Wizara imepata kibali cha kuajiri askari wapya 600 ambao watasambazwa kwenye maeneo hatarishi.
Masanja ameongeza kuwa Wizara itaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ili wananchi waweze kujikinga na wanyamapori hao.
Katika hatua nyingine, Masanja ameelekeza askari wanyamapori wa nyanda za juu kusini kuweka kambi katika kata ya Mbati na Marumba zilizopo Tunduru Kusini ambako tembo wameweka kambi kwa muda mrefu ili wawarudishe hifadhini.
Kuhusu suala la malipo ya kifuta jasho/machozi, Masanja amewataka wabunge kushirikiana na Serikali kuhakikisha orodha za wenye madai zifike Wizara ya Maliasili na Utalii kwa wakati ili malipo yaweze kufanyika kwa haraka.