Jeshi la Polisi nchini, limeendelea kushirikiana na watalaam mbalimbali katika kupambana na majanga ya moto hapa Nchini ambapo Taasisi isiyo ya kiserikali ya Sukos kova foundation imetoa mafunzo katika chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam – DPA, wakilenga kuwaongezea maarifa maafisa wa Jeshi hilo katika kukabiliana na majanga ya moto.
Akiongea mara baada ya mafunzo hayo kamishna wa Polisi mstaafu Suleiman Kova amesema Taasisi hiyo inajihusisha na kutoa mafunzo maalum ya kupambana na majanga na maafa ambapo amebainisha kuwa kutokana na mabadiliko ya sheria ya majanga Jeshi hilo linakiwa kuwa mstari wa mbele kukabiliana na majanga.
Ameongeza kuwa wametoa mafunzo hayo kwa maofisa hao wanafunzi ambao wametoka Tanzania bara na Zanzibar huku akibainisha kuwa anaamini Jeshi la Polisi na wananchi watanufaika kwa mafunzo yaliyotolewa na Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam Kamshna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Dkt. Lazaro Mambosasa ameishukuru Taasisi ya Sukos Kova Foundation kwa kutoa mafunzo hayo ambayo yanakwenda kunufaisha Taifa katika kukabiliana na majanga.
Amesema, maofisa hao wanatoka maeneo mbalimbali nchini na watakwenda kuwafundisha wananchi na askari pindi watakapolimaza mafunzo yao na kupangiwa kazi maeneo tofauti tofauti na Mkuu wa Jeshi hilo, huku Mwanafunzi wa kozi ya uofisa, Sarafina Chamlonde akisema mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi huku akieleza kuwa mafunzo hayo yamewaongezea mbinu na maarifa mapya katika kukabiliana na majanga ya moto.