Scolastica Msewa, Msata – Pwani.
Jumla ya Vijana 3,095 wamehitimu mafunzo katika shule ya awali ya kijeshi ya Kihangaiko Msata Mkoani Pwani na kuwa Askari wapya wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ambao watasambazwa kwenye vikosi mbalimbali nchini.
Akizungumzia mara baada ya Askari hao kula kiapo cha utii kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Meja Jenerali Jacob Mkunda, Mkuu wa Utumishi wa JWTZ, Meja Jenerali Marco Gaguti aliwataka kuzingatia utiii kanuni za kijeshi na kuheshimu maelekezo yote yanayotolewa na Viongozi wa nchi.
“Leo mnahitimisha mafunzo ya askari wapya katika shule hii ya Kihangaiko mnakuwa askari wapya wa JWTZ jeshi ambalo lina maadili na miiko yake, kazi kuu ya jeshi ni ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nataka kuwakumbusha kwamba jasho lenu na kazi yenu iwe ni kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maisha yenu yote,” alisema.
Gaguti aliongeza kuwa, “jukumu letu liwe ni kuhakikisha amani na utulivu inatamalaki ili Tanzania izidi kupiga hatua za maendeleo, nmekula kiapo ambacho mtaishi nacho katika maisha yenu yote kama Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni wajibu wetu kumtii rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu.”
Naye Kaimu Mkuu Shule ya Awali ya Mafunzo ya Kijeshi ya Kihangaiko, Meja Haji Suluhu Haji aliwataka wahitimu hao kuwa waaminifu, waadilifu na hodari katika kujenga Taifa kwa amani kiakili na kimwili ambapo askari hao walifanya maonesho mbalimbali waliopatiwa shuleni hapo ikiwamo namna ya kukabiliana na adui katika eneo la vita na mazoezi ya kuhimiri maadui.
Jumla ya askari 3095 wamehitimu mafunzo hayo ya awali ya kijeshi ambao ni kundi la namba 42 kwa mwaka 2020/2023 wakiwa tayari rasmi kutumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambapo wengine kadhaa walishidwa kuendelea na mafunzo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kifo.