Jeshi la polisi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetumia silaha za moto kuwatawanya waandamanaji na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Waandamanaji walikuwa wanafanya maandamano yaliyoratibiwa na viongozi wa Kikatoliki katika mji mkuu wa Kinshansa.
Katika maandamano hayo yanayopinga uamuzi wa Rais Joseph Kabila kuendelea kubakia madarakani hadi Disemba mwaka huu yamesababisha kukamatwa kwa watu kumi na tano jana ambapo kati yao watatu ni viongozi wa Kikatoliki, kwa mujibu wa Reuters.
Muhula wa utawala wa Rais Kabila ulikamilika mwaka 2016 kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo lakini ameendelea kubakia madarakani akieleza kuwa hali ya usalama imesababisha mazingira magumu ya kuitisha uchaguzi.
Viongozi wa kanisa katoliki na baadhi ya makanisa wameitisha maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika baada ya watu kutoka katika ibada ya Jumapili.