Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, umesema umekuwa ukipokea simu nyingi zinazoulizia kuhusu kuchomwa moto kwa kanisa moja katika dayosisi hiyo taarifa ambazo zimeleta taharuki.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, imesema kuwa hakuna kanisa lolote lililochomwa moto.
“Taarifa hizi zimeleta taharuki miongoni mwa waumini wetu na wananchi kwa ujumla. Napenda kutoa taarifa hii, ili kwa njia hii kupunguza usumbufu wa kuulizwa ulizwa kwa simu ya jambo hili.” Amefafanua Askofu huyo
Na kuongeza kuwa “Hakuna kanisa lolote la dayosisi hii lililochomwa moto. Pia hatuna taarifa zozote toka polisi wala mamlaka yoyote zinazoeleza uwepo wa nia au mazingira ya kuchoma moto kanisa letu.”.
Amesema wanazo taarifa za kimaungano, zilizowafikia kuwaeleza kuwa kuna mtu mmoja amekuwa anatumia nafasi yake kuwashawishi vijana wafanye fujo au kuchoma moto kanisa kwa sababu ambazo hawajajulishwa.
“Vijana hawa walikataa mpango huo, kwa kuwa mtuhumiwa ni mtu mwenye nafasi ya muhimu katika jamii, tumeamua kuijulisha mamlaka yake ya kinidhamu aonywe kusudi asivuruge uhusiano mwema wa kihistoria kati ya kanisa na mamlaka anayotumikia, tunaamini akumulikaye mchana, usiku anaweza akakuchoma.” Amesema Bagonza
Na kuongeza kuwa “Kwa kuwa mtuhumiwa huyo mchochezi ni muumini wa kilutherani, tunapenda kumuonya aache. Kama hataki kuacha uchochezi, basi yeye mwenyewe achome kanisa kuliko kusingizia watu wengine wasiokuwepo”.