Askofu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Joseph Gwajima ambaye miezi kadhaa iliyopita sauti iliyosadikika kuwa yake ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuleta tafrani kwa kile alichokizungumza huku kikitafsiriwa kuwa ni matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, amekana mashitaka yanayomkabili mahakamani.

Akisomewa mashitaka jana (Julai 20) katika mahakama ya Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Wilfred Dyansobera, Gwajima alikana maelezo yaliyotolewa na wakili wa Serikali, Joseph Maugo kuwa kati ya March 16 na 25 mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers , alimtolea matusi Mwadhama Polycarp Pengo kwa kumuita mtoto, mpuuzi na hana akili.

Ingawa Gwajima alikana kumshambulia Kadinali Pengo, alikiri kuwa yeye ndiye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na kwamba aliitwa polisi Machi 27 mwaka huu kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 8 mwaka huu baada ya kuelezwa kuwa mshitakiwa mmoja kati ya washitakuwa watatu wa kesi hiyo hakuwepo na kwamba kwa mujibu wa sheria mshitakiwa huyo alitakiwa kuwepo mahakani hapo.

Katika kesi hiyo, pia Gwajima anashitakiwa kwa kosa la kushindwa kuhifadhi vizuri silaha na risasi anazomiliki kihalali.

Washitakiwa wengine akiwemo mlinzi wa Gwajima, George Mzava, Yekonia Bihagaze na Mchungaji Georgey Milulu, wao wanashtakiwa kwa kosa la kumiliki bastola na risasi 20 kinyume cha sheria.

Ronaldinho Gaucho Awaomba Radhi Mashabiki
Chadema Yamfungulia Mlango Lowassa Kiroho Safi, Dr. Slaa Azungumza