Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imesema Askofu Josephat Gwajima hatakiwi kuhudhuria mikutano ya Bunge miwili au isiyopungua mitatu mfululizo kutokana na utovu wa nidhamu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Emmanuel Mwakasasa ametoa kauli hiyo wakati akisoma ripoti ya kamati yake leo Agosti 31, Bungeni jijini Dodoma baada ya vikao viwili vilivyokaa kumsikiliza Askofu Gwajima wiki iliyopita.
Mwakasasa amesema kuwa Shahidi huyo alikiri kuwa kauli zote ni zake kwa asilimia 100 na akasema kuwa alikua anahubiri hivyo kamati haina haki ya kuhoji juu ya mahubiri na kutokana na kanuni za Bunge Mhe.Gwajima ana hatia.
Kutokana na shuhuda kukiri kuwa zote ni kauli zake, kamati imejiridhisha kuwa hakuna mahubiri ambayo yanatakiwa kufanyika kwa kukiuka sheria za nchi hivyo kauli hiyo haiwezi kuwa kinga ya kukwepa kuhojiwa na kutiwa hatiani.
Aidha kamati hiyo katika ripoti yake imesema kuwa Askofu Gwajima ameonyesha utovu wa nidhamu katika siku zote mbili za Mahojiano kwa kukataa kutumia vifaa alivyoandaliwa na kukataa kujibu kwa ufasaha maswali aliyokuwa anaulizwa kwa kuiaminisha kamati kuwa alikua anahubiri.
Askofu Josephat Gwajima anatuhumiwa na Kamati ya Haki, maadili na Madaraka ya Bunge kwa makosa ya kuchonganisha Muhimili wa Bunge na Serikali, au Serikali na Wananchi kutokana na kauli zake ambazo amekua akizitoa hadharani za kutatiza juu ya Chanjo ya Corona na Uingiaji wake nchini Tanzania.