Mbunge wa jimbo la Kawe, Askofu Josephat Gwajima amesema jicho lililomuona Dkt. Philip Mpango anafaa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni la juu sana.

Askofu Gwajima amesema hayo alipokuwa akizungumza katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa tatu wa Bunge jijini Dodoma, mara baada ya jina la Dkt. Mpango kupendekezwa kwa ajili ya kupigiwa kura na Wabunge, ili kuthibitishwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

“Tumezoea kuwanukuu Wanafalsafa mbalimbali Duniani, lakini leo nataka nimnukuu Mtanzania mmoja anayeitwa Pierre Liquid niseme Mama Samia ni Konki Fire na Mama Samia yupo juu yupo Mawinguni, na ndio maana amefanikiwa kumteua Mpango kuwa Makamu wa Rais,” amesema Gwajima.

Gwajima amempogeza Dkt. Mpango kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania akimuelezea kama mtendaji na mtekelezaji wa mambo na kutoa mfano wa jinsi Dkt. Mpango alivyoshughulikia changamoto ya bandari ya majahazi yanayotoka Zanzibar katika eneo la Mbweni jimboni Kawe ambayo ilikuwa haijafunguliwa kwa kipindi kirefu.

Dkt. Mpango amepitishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ataapishwa kesho Machi 31, 2021, Ikulu Jijini Dodoma.

Ombi la BAVICHA kwa Rais Samia
Makamu wa Rais: Bunge lampitisha Dkt. Mpango kwa 100%, kuapishwa kesho