Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es salaam, Dkt. Valentino Mokiwa amegoma kujiuzulu wadhifa huo akidai kuwa mwenye uwezo wa kumfuta nafasi hiyo ni Sinodi ya Dar es salaam ambayo ndiyo mwajiri wake na si mtu mwingine.
Amesema kuwa, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Dkt. Jacob Chimeledya au Askofu mwingine yeyote wa kanisa hilo hawawezi kumfuta wadhifa huo.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Mokiwa amesema kuwa uamuzi wa Askofu Chimeledya kumvua wadhifa huo hauna uhalali wowote, pia ameshauriwa vibaya na washauri wake.
“Pamoja na mambo ninayofanyiwa lakini nimewasamehe kwa yote kwani taasisi za dini hazipaswi kufanya mambo ya aina hii, nawaomba viongozi wa dini tuache kutengeneza migogoro, nikiwa Askofu Dayosisi hii nimefanya mambo mengi sana makubwa, lakini hatua aliyokuja nayo Askofu Mkuu umetokana na ushauri mbaya,”amesema Askofu Mokiwa.
Hata hivyo,Askofu Mokiwa amesema kuwa mbali na kushauriwa vibaya kwa Askofu Mkuu,pia kumeonekana kuwepo kwa makundi ndani ya kanisa kwa kutoa siri za ofisi.