Mlinda mlango wa Chelsea Asmir Begovic kwa mara la kwanza amezungumzia tofauti ilizopo kati ya aliyekua meneja klabuni hapo Jose Mourinho na meneja wa sasa Antonio Conte.
Begovic, mwenye umri wa miaka 29, alisajiliwa na Jose Mourinho mwaka 2015, akitokea Stoke City, baada ya kumkuna meneja huyo kutoka nchini Ureno.
Begovic amesema kuna tofauti kubwa kati ya Conte na Mourinho, na jambo hilo limekua chachu ya mabadiliko yanayoonekena kwa sasa ndani ya kikosi chao.
Mlinda mlango huyo kutoka Bosnia na Herzegovina amesema utendaji kazi wa Conte umekua sababu ya mabadiliko makubwa yaliopo kikosini kwa sasa, na anaamini hali hiyo itafanikisha furaha itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Amesema meneja huyo kutoka nchini Italia, ana desturi ya kumnoa mchezaji kwa kumuelesha taratibu mpaka aelewe, tofauti na ilivyokua kwa Mourinho, ambapo wakati mwingine alionekana kutumia kauli nzito kumuelesha mchezaji.
“Kwa kweli Conte ni mtu wa kipekee katika ufundishaji wake, yupo tayari kupoteza muda wake kwa ajili ya kumuelimisha mmoja baada ya mwingine, na atajiridhisha kama kweli mmemuelewa kwa vitendo. ‘Sidhani kama tunapaswa kumuangusha katika utendaji wake.”
“Hapendi kutuona tukiwa katika hali ya simanzi kabla na baada ya mchezo, jambo hilo kwake ni mwiko na muda wote hututaka tuwe na furaha na kuelekeza akili zetu mchezoni.”
“Kwa sababu hizo, kuna tofauti kubwa sana na ya Conte na Mourinho ambaye aliachana nasi mwishoni mwa mwaka 2015.” Alisema mlinda mlango huyo chaguo la pili.”
Chelsea ya Antonio Cote kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi ya nchini England kwa tofauti ya point tisa, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Arsenal mwishoni mwa juma lililopita.
Mwishoni mwa juma hili The Blues watapambana na Burnley na kama watafanikiwa kushinda, watafikisha idadi ya michezo 20 waliyochomoza na point tatu muhimu kwa msimu huu wa 2016/17.