Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imezindua safari kutoka Uwanja wa Ndege wa Chato mkoani Geita hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.

 Akizungumza wakati wa uzinduzi wa safari hizo ,Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi amebainisha kuwa, safari zitaanza  rasmi Januari 9 mwakani na kutakuwa na safari mbili kwa wiki kwa siku za Alhamisi na Jumamosi.

Matindi amewambia waandishi wa habari kuwa, kuanza kwa safari hizo kunatimiza azma ya ATCL kufikisha huduma kila eneo la nchini.

“Kuanzisha safari hizi tumeangalia mambo mengi ikiwemo uwezo wa uwanja wa ndege ambao una kilometa tatu ambazo zinakidhi kigezo cha kupokea ndege kubwa zikiwemo airbus na dreamliners,” amesema Matindi.

Matindi amesema safari hizo zitawapunguzia wananchi wakiwemo wafanyabiashara wa Geita tatizo la kutembea zaidi ya kilometa 200 kwenda Mwanza na Bukoba kufuata huduma hiyo.

“Pia tumelenga kukuza sekta ya utalii kwani uwanja upo karibu na hifadhi za Burigi Chato na Rubondo na tumelenga abiria wa nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda ambao ni majirani zetu, kwani baadaye tumenuia kufanya safari zetu mara tatu kwa wiki kutokea Chato kupitia Kahama na Mwanza hadi Dar es Salaam,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema safari hizo zitaongeza fursa na kuchagiza maendeleo ya kiuchumi pia Ameyakaribisha mashirika mengine ya ndege ndani na nje ya nchi kuanzisha safari kutokea uwanja huo kwani mkoa una miundombinu rafiki kupokea wageni kutoka mataifa yote.

Mgombea urais wa upinzani akamatwa
Argentina yapitisha muswada unaohalalisha utoaji wa mimba

Comments

comments