Mkuu wa kitengo cha mawasiliano – ATCL, Josephat Kagirwa amesema kampuni hiyo imeanzisha mpango wa “kibubu” utakaowawezesha wananchi kulipia kidogo kidogo mpaka atakapo kamilisha malipo ya tiketi yake ya ndege.
Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo septemba 9, 2021 Jijini Dar es Salaam ambapo amesema mpango huo utawawezesha wananchi kupangilia safari zao kwa kulipia tiketi zao kidogo kidogo.
Amesema kuwa katika mpango huo, mwananchi atatakiwa kuweka Sh50,000 kwa mara ya kwanza na kiasi kinachobakia atatakiwa kulipa kidogo kidogo kwa kiwango anachokimudu mpaka safari yake itakapofika.
“Tumeweka mpango huu ili kuwasaidia wananchi kuweka fedha kidogo kidogo ili kulipia tiketi ya ndege ndani ya muda ambao amepanga kusafiri,” amesema Kagirwa.
Kwa upande wake, meneja wa mtandao wa safari na usimamizi wa mapato katika kampuni hiyo, Edward Nkwabi amesema kwa kuanzia wananchi watafanya malipo ya awali ya tiketi zao (booking) katika ofisi za ATCL lakini baadae wataweza kulipia kwa njia ya benki.