Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) limeanza kusafirisha mizigo nje ya nchi baada ya kusitisha safari zake za abiria kwenda nje ya nchi kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa covid -19.
ATCL jana imeanza safari yake ya kwanza ya kusafirisha mizigo kwenda visiwani Comoro kwa kubeba bidhaa za matunda na mbogamboga.
Akizungumza na TBC , Afisa mauzo na mizigo wa shirika hilo, Innocent Swai amesema kuwa wameamua kuendeleza shughuli zao kwa njia hiyo ya kusafirisha mizigo ili kuendeleza mahusiano na nchi zenye uhitaji na huduma zao.
Amesema wamejipanga vizuri na kwa kuanza wanatumia ndege ndogo ambayo ina uwezo wa kubeba hadi tani kumi za mizigo na kila siku za alhamis itakuwa inapeleka mizigo Comoro.
Aidha amebainisha kuwa baada ya wiki mbili wataanza safari kwenda kupeleka na kuchukua mizigo India Safari nyingine wataifanya China ya kupeleka bidhaa zinazopatikana baharini kama samaki.