Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), kupitia ndege yake aina ya Air Bus 220-300 imeanza safari ya kuelekea jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Demokrasi ya Congo kupitia Ndola nchini Zambia.
Akizindua safari hiyo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amesema safari hiyo inakwenda kufungua zaidi biashara na utalii baina ya Tanzania na Congo kutokana na nchi hiyo kutegemea zaidi bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yake.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi, amesema safari ya Lubumbashi kupitia Ndola itafanyika mara tatu kwa wiki ambapo amesema mahitaji ya soko la Lubumbashi kuwa ni ya kuridhisha ikichagizwa na wafanyabiashara wa nchi hiyo kutumia uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kuelekea nchini China kibiashara.
Kwa upande wa wasafiri baadhi yao wamesema kuwa safari hiyo inakwenda kurahisisha biashara kutokana changamoto iliyokuwa ikiwalazimu kupitia Nairobi.
Ndege aina ya Airbus ina uwezo wa kubeba abiria mia moja thelathini na mbili (132) kutoka Dar es Salaam.