Shirika la ndege la Tanzania, (ATCL) limeanza Safari yake ya kwanza leo kuelekea Johannesburg nchini Afrika Kusini kwa kutumia ndege yake aina ya Airbus 220-300 ambayo inatarajia kufanya safari zake mara nne kwa wiki kwa siku ya Ijumaa, Jumapili, Jumatano na Jumatatu.
Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Mhandisi Ladslaus Matindi leo wakati wa uzinduzi wa safari ya kutoka Dar es salaam kwenda Johanesburg ambayo imeanza rasmi Ijumaa ya leo ya Juni 28, 2019.
”Ndege ya ATCL aina ya Airbus 220-300 imeondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam Tanzania (JNIA) saa 4:30 asubuhi ikitarajia kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa OR Tambo, Afrika Kusini saa 6:45 mchana”.
Mbali na safari hiyo ambayo imezinduliwa leo, amesema Air Tanzania itaendelea kuzindua safari nyingine nyingi duniani ambapo baada ya uzinduzi huu amesema safari inayofuata ni ya kwenda India katika mji wa Mumbai ambapo wanatarajia kufanya safari hii mara tatu kwa wiki lakini pia safari ya China inatarajiwa kuanza katika mji wa Guangzhou.
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema lengo la kuanzishwa kwa safari hiyo ni kupunguza muda wa safari kwani abiria walikuwa wanaunganisha ndege ili kufika Afrika Kusini.
Kwandikwa ameongeza kuwa safari hii pia itasaidia kuboresha mahusiano ya kidiplomasia baini ya nchi hizi mbili.