Mamlaka za Serikali Nchini Cameroon, zimesema Mvua kubwa iliyonyesha katika mji mkuu wa Yaounde imesababisha mafuriko makubwa na kuua takriban watu 28, huku wengine wakiwa hawajulikani walipo na shughuli za uokozi zikiendelea kufanyika.
Maporomoko hayo ya Ardhi yaliyotokea katika Wilaya ya Mbankolo iliyopo Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, yaliharibu na kusomba takriban nyumba 30, huku Waokoaji wakisema wamepata miili 23 katika matope na vifusi huku tukio hilo likikumbusha Mwaka wa 2019, ambapo watu wapatao 43 waliuawa katika tukio kama hilo katika mji wa Magharibi wa Bafoussam.
Wamesema, hali si shwari katika eneo hilo licha ya kuwa bado wanaendelea na zoezi la kuwatafuta manusura, lakini wakaonya kuwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka kutokana na uhalisia wa hali ilivyo mara baada ya maporomoko kutokea.
Hata hivyo, inaarifiwa kuwa Maporomoko hayo ya ardhi ni ya kawaida jijini Yaounde wakati wa msimu wa mvua na Nyumba nyingi zilizosombwa zilikuwa zinatarajia kubomolewa kutokana na ujenzi duni ambapo Novemba 2022, watu wasiopungua 15 walifariki katika maporomoko ya ardhi katika jiji hilo.