Mipango ya mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona ya kumnyakua mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Atletico Madrid Antoine Griezmann imeingia gizani, baada ya mchezaji huyo kusaini mkataba mpya.

Kwa muda wa majuma kadhaa Griezmann alikua akihusishwa na taarifa za kuihama Atletico Madrid katika kipindi hiki, lakini uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake Wanda Metropolitano umefuta mpango huo, kufuatia kukamilisha azma ya kumsainisha mkataba mpya.

Taratibu za kusaini mkataba mpya kwa mshambuliaji huyo, zimefanywa nchini Urusi ambapo ndipo alipo kwa sasa, kwa ajili ya kuitumikia timu ya taifa lake la Ufaransa kwenye fainali za kombe la dunia.

Mtendaji mkuu wa Atletico Madrid Miguel Angel Gil Marin, alifunga safari hadi Urusi kukamilisha mpango huo, ambao umepokelewa kwa furaha na mashabiki wa Atletico Madrid ambao walionyesha kuchukizwa na harakati za Griezmann kuhusishwa na FC Barcelona.

Wakati Griezmann  akisaini mkataba mpya hadi mwaka 2023, hali kama hiyo imehitimishwa na beki wa kushoto wa Atletico Madrid Hernandez, baada ya kukubali kusaini mkataba mpya utakaomuweka klabuni hapo hadi mwaka 2024.

Mtendaji mkuu wa Atletico Madrid Miguel Angel Gil Marin, pia alikutana na mchezaji mpya wa klabu hiyo Thomas Lemar ambaye yupo kwenye kambi ya timu ya taifa ya Ufaransa, huko Urusi.

Lemar amesajiliwa na Atletico Madrid kwa ada ya Euro milioni 70 sawa na dola za kimarekani milioni 81.34 na ameweka rekodi ya kuwa mchezjai ghali katika histoaria ya klabu hiyo.

 

Serikali yapigilia msumari wa moto wanaokamatwa Serengeti
Timu ya Taifa ya Saud Arabia yanusurika na ajali ya Ndege