Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ wa Singida Fountain Gate, Mghana Enock Atta Agyei amesema licha ya kukaa nje muda mrefu, lakini mashabiki watarajie mambo makubwa kutoka kwake msimu ujao 2023/24.
Kiungo huyo wa zamani wa Azam FC amesaini dili la mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo baada kushindwa kuitumikia tangu Januari 2023, kufuatia kuchelewa kwa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka kwa waajiri wake wa zamani AC Horoya ya Guinea.
“Naipenda Tanzania na nafurahia nikiwa hapa. Nashukuru uongozi kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuonyesha uwezo wangu. Licha ya kutocheza muda mrefu ila haiwezi kuniathiri kwani muda mwingi nilikuwa nafanya mazoezi,” amesema.
Akimzungumzia mchezaji huyo, kocha mkuu wa Singida, Hans Van Der Pluijm amesema hana shaka juu ya uwezo wa nyota huyo.
“Ana spidi kubwa uwanjani. Anajua kukaa na mpira. Ana uwezo wa kuwasumbua wapinzani na kucheza namba 10 na 11. Hakuna kocha yeyote yule asingependa aina ya uchezaji wake kwa sababu anaongeza wigo mpana kwenye kikosi kilichopo,” amesema.
Singida iliyoweka kambi jijini Arusha kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ya ndani na nje, imekamilisha usajili wa nyota kadhaa wakiwemo Joash Onyanyo aliyetokea Simba SC, Nicolas Wadada na Yahya Mbegu kutoka Ihefu FC.