Zoezi la kumuaga rapa Nipsey Hussle kwenye ukumbi wa Staples Center jijini Los Angeles nchini Marekani lililofanyika jana liliambatana na tukio lingine la shambulizi la risasi lililosababisha kifo cha mtu mmoja.
Nipsey Hussle ambaye ameagwa rasmi na mamilioni ya watu duniani kote, aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa nje ya duka lake la Marathon katika viunga vya Los Angeles. Alipigwa risasi mara sita.
Kwa mujibu wa tweet ya Mkuu wa Idara ya Polisi ya Los Angeles, Michel Moore, watu wengine watatu walijeruhiwa baada ya watu waliokuwa kwenye gari moja kufyatua risasi kwenye mitaa ya jiji hilo, karibu na eneo la tukio la kumuaga Nipsey Hussle.
“Katikati ya zoezi la kumuaga Nipsey Hussle, kulikuwa na mashambulizi manne kwenye mitaa ya 103 Main. Wahanga ni wanaume watatu wenye asili ya Kiafrika na mwanamke mmoja, wenye umri kati ya miaka 30-50. Bahati mbaya mmoja alifariki dunia. Watuhumiwa waliokuwa kwenye gari aina ya Hyundai walifyatua risasi kuelekea kwa wahanga. Ni lazima tukomeshe vurugu hizi za kipuuzi,” Moore alitweet.
Kwa mujibu wa TMZ, umati wa watu uliojitokeza kumuaga kwa heshima rapa huyo, baadaye walienda katika mtaa ambao rapa huyo aliuawa, lakini walianza kutawanyika baada ya kusikia sauti ya milio ya risasi.