Mshambuliaji wa klabu ya Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang, ameendelea kuthibitisha kuwa mbioni kuihama klabu hiyo, kufuatia kauli aliyoitoa alipohojiwa na kituo cha redio cha nchini Ufaransa.

Mshambuliaji huyo raia wa nchini Gabon, anawaniwa na klabu kubwa barani Ulaya kama Real Madrid, Manchester United pamoja na Chelsea.

Katika mahojiano na kituo cha redio cha Ufaransa, Aubameyang, alisema anataka kucheza soka kwa kiwango kikubwa, na anaamini hakuna njia ya mkato ya kulifikia lengo hilo, zaidi ya kutafuta mahala ambapo patampa changamoto mpya.

“Kama ninahitaji kucheza kwa kiwango cha juu zaidi, itanihitaji kusaka mahala ambapo nitaweza kupata changamoto ya kukuza soka langu. Natambua Real Madrid bado wana ndoto za kunisajili, lakini pamekua na mlolongo mrefu mazungumzo yanayoendelea kupitia vyombo vya habari, Alisema Aubameyang. Ninaipenda Dortmund, lakini siwezi kusema nitakua hapa kwa zaidi ya miaka miwiwli ijayo. Inawezekana uongozi ukaniongezea mkataba lakini bado kuna uwezekano wa kulitafakari jambo hilo.”

Aubemayang ameshafunga mabao 70 katika ligi ya nchini Ujerumani (Bundesliga) tangu alipojiunga na Dortmund mwaka 2013 akitokea Saint-Étienne, na kwa misimu miwili mfululizo amekua mfungaji bora wa klabu.

Msimu uliopita alitangazwa kuwa mchezaji bora wa ligi ya nchini Ujerumani (Bundesliga).

Mshambuliaji huyo ambaye alizaliwa nchini ufaransa miaka 27 iliyopita, alikua sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Gabon kilichoshindwa kufurukuta katika fainali za Afrika za mwaka huu zinaoendelea nchini humo, baada ya kutolewa kwenye hatua ya makundi.

Zanzibar kuwa makao makuu ya kiswahili
Bunge lapitisha muswada wa marekebisho ya sheria