Tetesi za kuuzwa kwa mshambuliaji kutoka nchini Argentina na klabu ya Man City Sergio Kun Aguero itakapofika mwishoni mwa msimu huu, zimeenedelea kuchukua nafasi kubwa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini England.
Man City wamekanusha kuwepo kwa uwezekano wa kuondoka kwa mshambuliaji huyo, ambaye inadaiwa ameshindwa kumshawishi meneja Pep Guardiola, ili atumike katika kikosi cha kwanza.
Klabu hiyo ya Etihad Stadium, inadaiwa kuwa katika mpango wa kumsajili mshambuliaji kutoka nchini Gabon na klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani Pierre-Emerick Aubameyang.
Gazeti la The Sun limetoka na taarifa hiyo mapema hii leo, kwa kusisitiza kuna uwezekano wa biashara hiyo ikafanyika mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa za gazeti hilo zimeongeza kuwa, Man city wamejipanga kikamilifu katika ushindani wa kumsajili Aubameyang, ambaye pia anawaniwa na klabu za PSG, Real Madrid, FC Barcelona, Chelsea na Inter Milan.
Pauni milioni 40 zinadaiwa kutengwa kwa ajili ya usajili wa Aubameyang, na kama itashindikana klabu ya Man City itakua tayari kuongeza dau hilo, ili kukamilisha azma ya kumnasa mshambuliaji huyo ambaye pia ni nahodha wa timu yake ya taifa ya Gabon.
Juma lililopita Aubameyang alieleza dhamira ya kutaka kuondoka Westfalenstadion kwa kigezo cha kuhitaji changamoto mpya ya kucheza soka lake.
Kwa msimu huu wa 2016/17, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ameshaifungia Dortmund mabao 21 katika michezo 24 aliyocheza.