Imefahamika kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Kiungo Mshambuliaji mpya wa Simba SC, Muivory Coast, Aubin Kramo akafanyiwa oparesheni ya goti.
Muivory Coast huyo juma lililopita aliuomba uongozi wa Simba SC, uumpe ruhusa arejee kwao kwa ajili ya kutibiwa kabla ya kurudi nchini.
Kiungo huyo alijitonesha majeraha hayo ya goti katika moja ya mchezo wa kirafiki walioucheza wakati wakijiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa majibu ya madaktari yanatarajiwa kujulikana juma hili, licha ya kuwepo uwezekano mkubwa wa kufanyiwa oparesheni kiungo huyo.
Ahmed amesema kuwa kwa mujibu wa madaktari wa timu hiyo, jeraha hilo alitoka nalo klabu yake ya zamani ya ASEC Mimosas ya Ivory Coasta, lakini limejitokeza baada ya kutua Simba SC.
“Kramo anasumbuliwa na goti, huenda tatizo lake lilianzia akiwa ASEC Mimosas, lakini limekuja kujitokeza akiwa na Simba SC kwa siku chache ambazo amejiunga katika timu msimu huu.
“Tuwapongeze madaktari kwa kugundua kuwa kiungo huyo amekuja na jeraha hilo akitokea katika klabu yake ya zamani, na baada ya kuona hilo wakamuondoa kikosini kwa hofu ya kupata majeraha zaidi, kwani tungemtumia angepoteza ndoto zake za soka kutokana na ukubwa wa jeraha la kusumbuliwa na mishipa ya nyuma ya goti,” amesema Ahmed.