Wakati kikosi cha Simba SC kikiwa katika maandalizi ya mwisho ya mchezo wa kuwania kutinga Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ Aubun Kramo ameomba kurudi nyumbani kwao kwa matibabu.
Juma lililopita iliyopita mchezaji huyo aliumia goti kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Ngome FC, jeraha ambalo linatarajia kumweka tena nje kwa muda mrefu.
Akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini, Kramo alisema ameuomba uongozi wa timu hiyo ili kumruhusu arudi kwao Ivory Coast aende kutafuta tiba ya tatizo hilo la goti ambalo limekuwa likimsumbua tangu alipojiunga na timu hiyo miezi miwili iliyopita.
“Nasubiria majibu ya vipimo vya MRI ili kujua ukubwa wa tatizo lakini nimeuomba uongozi ikiwezekana waniruhusu niende nyumbani kupata tiba ya tatizo langu,” amesema Kramo.
Inaelezwa kuwa Kramo alishakutana na viongozi wa Simba SC na kuwaeleza ombi lake la kutaka kurudi nyumbani na viongozi bado wanafikiria kumruhusu mchezaji huyo arejee nyumbani kwao.
Inaelezwa viongozi wa Simba SC, wanaumiza kichwa juu ya mchezaji huyo kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara kitu ambacho kinasababisha ashindwe kuitumikia timu hiyo tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu.
Tangu ajiunge na Simba SC, Kramo ameichezea klabu hiyo mechi nne za kirafiki dhidi ya Power Dynamos aliyotokea benchi na mechi nyingine zakiafiki dhidi ya Kipanga FC, Comsmopolitan na Ngome FC ambazo zote alifunga.