Hatimaye Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na Klabu ya Bechem United Augustine Okrah amethibitisha ataitumikia klabu ya Simba SC ya Tanzania kwa msimu ujao, baada ya kukamilisha taratibu zote.
Okrah alikua akitajwa kuwa kwenye rada za Simba SC katika kipindi hiki cha usajili wa kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa, huku Uongozi wa Msimbazi ukishindwa kuthibitisha hilo.
Mshambuliaji huyo ambaye juzi Jumapili (Juni 26) alicheza mchezo wake wa mwisho akiwa na Bechem United amesema “Nitakuja Tanzania siku chache zijazo, naweza kusema kila kitu kimekwenda vizuri, unajua kama mchezaji unajisikia faraja ukifuatwa na klabu inayokuhitaji hadi ulipo, hii ni heshima kubwa.”
“Simba ni klabu kubwa ambayo kila mchezaji mwenye ndoto za kufika mbali angetamani kuitumikia, nimekuwa nikiifuatilia, ina mashabiki wengi wanaoipenda klabu yao, sina wasiwasi kuja kuitumikia klabu kubwa kama hiyo.”
Aidha Okrah anayenukia kuchukua tuzo ya Kiungo Bora wa Ligi Kuu ya Ghana amesema ujio wake ndani ya Simba anataka kuendeleza msimu wake bora akitokea Bechem.
“Kabla ya yote mimi ni mchezaji ambaye najitambua, nafahamu nakwenda Simba ambayo ni wazi nitakutana na wachezaji wakubwa lakini nitatumia kipaji changu na juhudi zangu kupata nafasi, mimi sio mchezaji nitakayekubali kirahisi ushindani wa nafasi,” amesema.
Ingawa Simba inafanya siri usajili huo, lakini Okrah aliyefunga mabao 14 katika mechi 31 akiwa na ‘The Hunters’ anakuwa staa wa pili kumalizana na wekundu hao akitanguliwa na mshambuliaji kutoka Zambia Moses Phiri aliyesaini mkataba wa miaka miwili.