Mamlaka ya Maji Arusha (AUWSA) imetakiwa kuharakisha zoezi la tathmini ya kupeleka huduma ya maji katika Mji wa Namanga ili kusaidia wananchi kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji.
Agizo hilo limetolewa na naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati wa ziara yake kwenye chanzo cha mradi wa maji wa Longido katika mto Simba uliopo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kujionea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wake.
Mhandisi Sanga alisema ameridhika na hatua aliyoishuhudia ya ujenzi wa mradi wa Longido lakini ameitaka AUWSA kuhakikisha inatazama namna ya haraka ya kufikisha huduma ya maji kwenye mji wa Namanga kutoka kwenye chanzo cha mradi huo hasa ikizingatiwa kwamba mji huo unasumbuliwa na kero ya upatikanaji wa huduma ya maji.
“Ninawapongeza AUWSA kwa usimamizi mzuri wa mradi lakini nataka kuona mnafanya tathmini haraka ya namna ya kufikisha maji kwenye mji wa Namanga kwani kuna changamoto kubwa sana kwenye mji huo,” amesema Mhandisi Sanga.
Akizungumzia uwezekano wa kutumia chanzo hicho cha mto Simba kupelekea maji Namanga, Mhandisi Sanga alisema maji yaliyopo yanaonekana kuwa mengi na yanaweza kutosheleza kuhudumia maeneo yote mawili sambamba na maeneo mengine ya jirani.
“Tumekuja hapa kuona uwezekano wa kutoa maji kwenye eneo hili ili kufikisha Namanga, na nilichoshuhudia ni kwamba chanzo hiki kinaonekana kuwa na maji ya kutosha kwa maeneo yote mawili yani Longido na Namanga,” alisema.